UGONJWA WA SUGU WA FIGO -CHRONIC KIDNEY DISEASE (CKD)

Je umewahi kusikia mtu akisema figo zimefeli au zimeshindwa kufanya kazi? Hili ni jambo gani,figo kufeli? Katika mada hii tutalitazama ... thumbnail 1 summary



Je umewahi kusikia mtu akisema figo zimefeli au zimeshindwa kufanya kazi? Hili ni jambo gani,figo kufeli? Katika mada hii tutalitazama tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kabisa,au figo kufeli. Tutaangalia ni kitu gani na linatokeaje,nani huwa katika hatari ya kupata ugonjwa,madhara na jinsi mtu awezavyo kuepuka tatizo.

Ugonjwa sugu wa figo pia huitwa ugonjwa wa figo kushindwa kufanya kazi kabisa na hutokana na kuharibika kwa figo ndani ya muda mrefu kupita. Ni kitendo cha figo kupoteza ubora wake hatua kwa hatua hadi kufikia kiwango cha kutofanya kazi kabisa. Figo zinaposhindwa kufanya kazi majimaji yaliyochanganyika chumvi chumvi na madini na uchafu hukusanyika na kujijenga mwilini.

Katika hatua za mwanzo,ugonjwa wa kudumu wa figo huwa hauoneshi dalili,hadi pale figo zitakapofikia kufikia hatua ya kushindwa kabisa. Inafahamika kuwa tiba ya ugonjwa huu huelekezwa kwenye kuondoa dalili za ugonjwa,kwa sababu ni ugonjwa usioweza kutibika katika hatua za mwisho. Kwa mfano katika hatua ya tano mgonjwa mwenye ugonjwa sugu wa figo,huhitaji njia za ziada kama dayalisisi na kupandikiza figo ili mgonjwa aweze kuendelea kuishi.  Hebu tuanze sasa kwa kutazama dalili za ugonjwa sugu wa figo.



Dalili Za Ugonjwa Wa Figo Kufeli



Dalili za ugonjwa sugu wa figo si rahisi kuzitambua,kwa sababu katika hatua za awali,dalili huwa hazionekani wala kutambulika. Dalili za ugonjwa sugu wa figo huonekana wazi paleugonjwa unapofikia hatua isiyoweza kurudia hali ya kawaida. Yaani dalili huonekana pale ugonjwa unapokuwa katika hali isiyopona kabisa. Dalili hizo huweza kuwa zifuatazo:

-Kichefuchefu

-Kutapika

-Kupoteza hamu ya kula

-Mwili kuwa dhaifu na mchovu

-Kukosa usingizi

-Kupungua kiwango cha mkojo

-Miguu kujaa na kuvimba

-Miwasho isiyoisha

-Misuli kubana

-Maumivu ya kifua-husababishwa na mrundikano wa maji kwenye kuta za moyo

-Kupumua kwa shida-maji yanaporundikana kwenye mapafu

-Shinikizo la juu la damu


Chanzo Cha Ugonjwa Sugu Wa Figo



Ugonjwa sugu wa figo hutokea pale tatizo lolote au ugonjwa wowote unaposababisha figo kuharibika. Madhara ya figo kuharibika huanza pole pole na kuongezeka hadi pale inapofikia hali ya kushindwa kupona kabisa. Ugonjwa huanza na kudumu kwa miezi au miaka kadhaa. Baadhi ya magonjwa au matatizo ya kiafya yanayoweza kupelekea mtu kupata ugonjwa wa kudumu wa figo kuharibika kabisa ni kama yafutayo:

-Kisukari aina ya 1 na 2

-Shinikizo la juu la damu

-Glomerulonephritis

-Interstitial nephritis

-Polycystic kidney disease



Nani Yuko Kwenye Hatari Ya Kupata Ugonjwa Figo Kuharibika Kabisa?


Baadhi ya matatizo ambayo huweza kupelekea mtu kupata ugonjwa wa muda mrefu wa figo,kama mtu akiwa nayo ni pamoja na:

-Kisukari

-Shinikizo la juu la damu

-Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu

-Kuvuta sigara

-Unene kupita kiasi

-Kuwa na historia ya magonjwa ya figo katika familia

-Kuwa na umri mkubwa



Madhara Ya Ugonjwa Wa Muda Mrefu Wa Figo



Madhara ya muda mrefu ya ugonjwa wa figo ni kama yafuatayo:

-Mwili kujaa maji na kupelekea miguu,mikono na mapafu kuvimba. Pia huweza kupelekea shinikizo la juu la damu

-Potasium kuongezeka kwenye damu na kupelekea madhara katika utendaji kazi wa moyo,na huweza kusababisha kifo

-Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu

-Mifupa kuwa dhaifu na kuvunjika

-Anemia

-Kupungua hamu ya tendo la ndoa,jogoo kushindwa kuwika na kuwa mgumba

-Madhara kwenye mfumo wa kati wa fahamu,hali inayoweza kupelekea kukosa utulivu na kuzimia

-Kupungua uwezo wa kinga na hivyo kuwa katika hatari ya kupata magonjwa kwa haraka

-Hatari kwa wajawazito



Jinsi Ya Kuzuia Ugonjwa Wa Figo Kushindwa



Kwa kuwa ni ugonjwa usio na tiba tofauti na dayalisisi na kupandikiza figo nyingine,ni muhimu sana kujikinga ili kuepuka kupata tatizo hili. Swali linabaki nini kifanyike? Hebu tutazame hapa kidogo mambo ya kufanya:

-Epuka ugonjwa wa Kisukari na Shinikizo la damu. Haya ndiyo magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha figo kufeli. Kwa hiyo chukua tahadhari mapema,na jitahidi kupata tiba haraka akdri iwezekanavyo kwa magonjwa haya.

-Chakula. Kula matunda,mboga  za majani,nafaka nzima,nyama zenye mafuta kidogo sana na samaki. Hivi vitakusaidia kuweka msukumo wako wa damu katika msawazo na kukuepusha na shinikizo la juu la damu.

-Fanya mazoezi. Mazoezi yatakusaidia kuepukan ana magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu. Mwone daktari wako akupangie mazoezi yanayokufaa wewe.

-Epuka pombe na madawa mengine ya kulevya. Hii itakusaidia kupunguza sumu na uchafu ndani ya figo.


Ndugu msomaji,huu ni mwisho wa mada hii. Mada zilizopita tumetazama magonjwa ya figo-ugonjwa wa figo wa ghafula na Ugonjwa wa mawe kwenye figo. Mada itakayofuata tutaangalia Ugonjwa Wa Mwili Kuvimba (Nephrotic syndrome). Huu ni ugonjwa mwingine wa figo. Endelea kufuatana nasi.

Unaweza kupata virutubishi tiba kwa ajili ya afya ya figo zako. Dawa hizi zitakusaidia kuimarisha figo zako,ili uweze kuepukana na magonjwa mbali mbali ya figo. Wasiliana nasi kupitia afyagreen@gmail.com au tupigie kupitia +255 673 923 959.